Thursday, 28 August 2014

JUKWAA LA KATIBA TANZANIA LATOA TATHIMINI YA WIKI MBILI YA MWENENDO WA BUNGE MAALUMU LA KATIBA KUANZIA TAREHE 11-23 AGOSTI2014


Kaimu Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Hebron Mwakagenda.

JUKWAA la Katiba Tanzania (Jukata), limemtaka Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba Samuel Sitta kufuata sheria na kaanuni za bunge hilo.Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Kaimu Mwenyekiti wa Jukata,  Hebron Mwakagenda alisema kuwa kwa sasa Sitta hana mamlaka ya kukusanya maoni kwani ni kinyume na sheria ya tume ya mabadiliko katiba.
“Tumeshuhudia bunge maalumu la katiba likiongozwa na mheshimiwa Sitta likiendelea kupokea maoni ya makundi mbalimbali wakiwemo wafugaji, waandishi wa habari na wasanii ambapo ni kinyume na sheria,” alisema.
Mwakagenda alifafanua kuwa hatua hiyo imekwenda kinyume cha sheria namba 9 (1) ambacho kinaeleza kazi za tume ya mabadiliko ya katiba ambayo ilikuwa na kazi ya kukusanya, kuchambua, kuandika taarifa na kuwasilisha kwenye bunge ambapo kazi yake ni kuipitisha kama ilivyo kwenye kifungu cha sheria namba 25.
Katika suala la uondoaji wa vifungu kwenye rasimu hiyo alisema rasimu imezingatia kero na malalamiko ya wananchi hivyo kuyaondoa ukilinganisha na mantiki inayoendelea bungeni ni sawa na kurekebisha katiba ya mwaka 1977 na kubaki na malalamiko kwa wananchi kuwa viongozi hawawajibiki.
Pia aliyataka makundi yanayopingana kwenda kwenyekikao kinachotarajiwa kufanyika Ikulu wiki hii kwa moyo mkunjufu na kwa kuzingatia maslahi ya taifa na si vyama vyao.
Hata hivyo alisema kuwa pamoja na juhudi za kuendeleza mchakato wa katiba mpya lakini mchakato huo hautokamilika na kutumika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Alifafanua kuwa hali hiyo imesababishwa na mwingiliano wa shughuli mbalimbali za kiserikali zikiwemo za uandikishaji mpya wa vitambulisho vya kupigakura katika mfumo mpya wa BVR.
Pia alisema kuwa kupanda kwa joto la uchaguzi kwa sasa pia inaweza kusababisha katiba kutopatikana kwani takribani wanasiasa wote wamegeukia kwenye uchaguzi na si kupatikana kwa katiba.
“Sisi kama Jukata tunashauri mchakato huu kuhairishwa hadi baada ya uchaguzi mkuu na kuanza tena januari 2016 ili kuokoa gharama za uchaguzi kwa kuunganisha na kufanyika chaguzi zote kwa mara moja,” alisema Mwakagenda.

No comments:

Post a Comment