Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (kushoto) akifuta machozi huku akiwa ameshika fomu za kuwania nafasi ya Uenyekiti wa Bazara la Wanawake wa Chadema (Bawacha) alizokabidhiwa na baadhi ya wanakwake makao makuu ya Chama hicho jijini Dar es Salaam jana.
Vigogo wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), watachuana katika kinyang’anyiro cha kuwania uenyekiti wa baraza hilo baada ya jana baadhi ya wanawake kujitokeza kumchukulia fomu Mbunge wa Kawe, Halima Mdee.
Mbunge huyo anaungana na Mbunge wa Viti Maalumu,
Chiku Abwao na wanachama wengine, Lilian Wasira na Sophia Mwakagenda
ambao nao wamesharejesha fomu kuwania nafasi hiyo inayoshikiliwa na
Suzan Lyimo.
Mwisho wa kuchukua na kurejesha fomu ni Agosti 30 na uchaguzi unatarajiwa kufanyika Septemba 11, mwaka huu.
Wanawake zaidi ya 30 kutoka Kinondoni, Kawe, Pwani
na Ubungo jana saa 5.20 asubuhi, walifika katika ofisi za Bawacha
jijini Dar es Salaam kumchukulia fomu Mdee wanayedai kuwa ndiye
anayestahiki kuliongoza baraza hilo kutokana na msimamo wake wa uongozi
wa kutotaka kuyumbishwa.
“Tumekaa na kutafakari ili kumpata mwanamke
atakayeweza kuliongoza baraza hili kwa kututoa hapa tulipo na kutupeleka
mbele zaidi, tumeona Halima Mdee anatufaa zaidi ndiyo maana tumeamua
kuja kumchukulia fomu,” alisema Felister Njau, Katibu Mwenezi wa Jimbo
la Kawe.
Huku akishangiliwa na wenzake alisema, “Tunakwenda
kumtafuta sehemu yoyote alipo ili tukamkabidhi hii fomu na tutamwomba
akubali ombi letu.”
Msafara wa wanawake hao wakiwa na fomu yao mkononi
ukiongozwa na Mwenyekiti wa Wazee Kata ya Kunduchi, Elefedina Mali
ulikwenda makao makuu ya chama hicho ambako walimkuta Mdee na kumkabidhi
fomu hiyo.
Aliwashukuru na kuwaomba wamvumilie kwani anahitaji muda wa kulitafakari ombi hilo.
Huku akibubujikwa na machozi, Mdee (pichani)
alisema; “Nimewaelewa naombeni nikajitafakari kwanza, nitawaeleza
nitakachoamua.” Wanawake hao pia walichangishana fedha Sh53,000
walizomkabidhi Mdee kwa ajili ya kurejeshea fomu hiyo.
No comments:
Post a Comment