STAILI
ile ile waliyotumia Yanga SC kumpata mshambuliaji Emmanuel Arnold Okwi
ndiyo ambayo klabu yake ya zamani, Simba SC inaitumia kumrejesha kundini
Mganda huyo.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari jioni hii mjini Dar es Salaam, Okwi amesema
kwamba amesaini Simba SC mkataba huru wa muda, baada ya Yanga SC kumpa
barua ya kusitisha mkataba naye jana pamoja na kumshitaki Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF).
Okwi
amesema ameamua kuomba kuichezea Simba SC kipindi hiki ambacho ana
matatizo na Yanga SC ili kulinda kipaji chake, kwa kuwa hata FIFA
haitaki mchezaji akae bila kucheza.
“Sasa wakati Yanga wanaendelea
na kesi yao, mimi ninaomba nichezee Simba SC ili kulinda kipaji changu.
Nimewaandikia barua TFF na FIFA pia na nina matumaini usajili wangu
utaidhinishwa, kwa sababu mimi si tatizo katika hili,”amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba
wamemsaini mchezaji huyo baada ya kupitia kwa kina suala lake na Yanga
SC na kugundua haki ipo upande wa mchezaji.
“Baada ya kulipitia suala lake
na Yanga kwa undani kabisa na vielelezo ambavyo mchezaji mwenyewe
ametupatia, tumejiridhisha tuko sahihi kumsaini ili acheze mpira
kunusuru kipaji chake kipindi hiki ambacho ana matatizo na Yanga
SC,”amesema Poppe.
Tayari Simba SC imetuma jina la
mchezaji huyo katika usajili wake TFF na ataungana na Mganda mwenzake,
Joseph Owino, Warundi Pierre Kwizera na Amisi Tambwe na Mkenya, Paul
Kiongera katika wachezaji watano wa kigeni.
“Tumewaandikia barua TFF kuomba
kumtumia mchezaji huyu kwa muda wakati kesi yake na Yanga inaendelea,
tumeambatanisha na barua yake ambayo yeye anatuomba kucheza kwetu
kulinda kipaji chake,”amesema Poppe.
Okwi aliichezea Simba SC tangu
mwaka 2009 kabla ya Januari mwaka jana kuuzwa kwa dola za Kimarekani
300,000 Etoile du Sahel ya Tunisia.
Etoile haikulipa fedha hizo
Simba SC na baadaye ikaingia kwenye mgogoro na Okwi, aliyedai hakulipwa
pia mishahara yake kwa miezi mitatu.
Okwi akawafungulia Etoile kesi
FIFA na akaomba wakati mgogoro wao unaendelea, aruhusiwe kuchezea timu
yoyote kulinda kipaji chake, ndipo akajiunga na SC Villa ya kwao.
Akiwa SC Villa ndipo aliposaini
Yanga SC Desemba mwaka jana na pamoja na mapingamizi yaliyoanzia ndani,
na baadaye klabu yake, Etoile- lakini Okwi aliidhinishwa kuichezea timu
hiyo ya Jangwani.
Okwi aliichezea Yanga SC mechi
11 na kuifungia mabao matano- lakini kuelekea mechi tano za mwisho za
Ligi Kuu msimu uliopita akaingia kwenye mgogoro na klabu hiyo.
Okwi alisusa kushinikiza
amaliziwe fedha zake za usajili na mgogoro wao umeendelea huku mchezaji
huyo akiwa amesusa tangu Machi, miezi minne tu baadaye tangu asajiliwe.
Vikao kadhaa vimekwishafanyika
baina ya Okwi na Yanga SC tangu hapo kutafuta suluhu ya suala hilo na
kikao cha mwisho leo baina ya mchezo huyo na Mwenyekiti wa klabu hiyo,
Yussuf Manji matokeo yake ni nyota huyo kurejea Msimbazi.
Kuhusu deni lao la dola 300,000
kumuuza mchezaji huyo Etoile, Poppe amesema haihusiani kabisa na
usajili wake huu wa sasa. “Ile kesi yetu ya madai ya fedha zetu kule
FIFA ilikwishamalizika na vielelezo vyote vilipelekwa, bado kutolewa
hukumu tu,” amesema.
No comments:
Post a Comment