Dirisha la usajili limefungwa msimu huu, habari kubwa ikiwa ni ya
Radamel Falcao kutua Manchester United na Danny Wellbeck kutoka Man U
kwenda Arsenal kwa mkataba wa muda mrefu.
Falcao ameingia Man U kwa mkopo wa msimu mzima na anaweza kusajiliwa
moja kwa moja baada ya kipindi hicho, huku usajili mzima kwa klabu za
Ligi Kuu ya England (EPL) ukifikia rekodi mpya ya pauni milioni 835.
Mchezaji huyo wa Colombia amesema kwamba atacheza kama beki wa kati,
licha ya kujulikana kwamba ni mshambuliaji wa kati, hali iliyokuwa
inawatia matumbo joto Wayne Rooney na Robin van Persie wanaocheza nafasi
hiyo. Atakuwa analipwa kati ya pauni 190,000 na 265,000 kwa wiki.
Old Trafford wamempata Falcao wa Colombia na Monaco kwa pauni milioni
sita, wakakamilisha usajili wa Daley Blind kutoka Ajax kwa pauni
milioni 13.8 wakati wamemuuza Welbeck kwa pauni milioni 16.
Mchezaji mwingine muhimu wa EPL, ambaye hata hivyo alishindwa
kuonesha makali, Alvaro Negredo wa Manchester City amepelekwa Valencia
ya Hispania kwa mkopo wa msimu mzima. United wanashikilia rekodi ya
usajili ghali zaidi Uingereza, baada ya kumpata Angel Di Maria wa Real
Madrid kwa pauni milioni 59.7.
Wachambuzi wa masuala ya fedha, Deloitte, wanasema kwamba Kocha wa
Manchester United, Louis van Gaal ametumia pauni milioni 150 kwenye
usajili na ndiyo rekodi kubwa zaidi kwa msimu kwa klabu yoyote ile.
Kusajiliwa kwa Falcao kumeshangaza wengi, kwani alitarajiwa kwenda
ama Real Madrid au Arsenal alikokuwa akihusishwa sana msimu huu kabla ya
dirisha kufungwa saa tano usiku wa Jumatatu hii.
City pia wamemruhusu mchezaji wa kimataifa wa England, Micah Richards
kujiunga kwa mkopo Fiorentina nchini Italia wakati mpachika mabao wa
United, Javier Hernandez ameenda kwa mkopo Real Madrid na kusema ndoto
yake imetimia.
Hull ndio walivunja rekodi ya kusajili wachezaji wengi zaidi katika
siku ya mwisho, kwani walipata wanne; mshambuliaji Abel Hernandez, Hatem
Ben Arfa, Gaston Ramirez na Mo Diame.
Crystal Palace wamevunja rekodi yao kwa kumsajili winga wa Wigan,
James McArthur kwa pauni milioni saba. Matumizi ya EPL yameongezeka
kutokana na pauni bilioni tatu zinazopatikana kwa klabu kwa matangazo ya
televisheni, zikiwa ni asilimia 70 zaidi ya mkataba uliopita.
Liverpool msimu huu wa usajili wametumia jumla ya £117, Chelsea
£91.3m, Manchester City £50m, Arsenal £82m, Southampton £74.9m wakati
wenyewe walipata £92m kwa kuuza wachezaji wao nyota sita.
Wachezaji wengine waliovunja rekodi ya usajili wa bei mbaya ni Alexis
Sanchez aliyetoka Barcelona kwenda Arsenal kwa £35m, Diego Costa kutoka
Atletico Madrid kwenda Chelsea kwa £32m, Eliaquim Mangala wa FC Porto
aliyekwenda Manchester City kwa £32m, Cesc Fabregas toka Barcelona hadi
Chelsea kwa £30m.
Wachezaji wengine ni Ander Herrera toka Athletic Bilbao kwenda
Manchester United kwa £29m, Romelu Lukaku aliondoka Chelsea na kujiunga
Everton kwa £28m, Luke Shaw kutoka Southampton hadi Manchester United
kwa £27m na dili linaweza kupanda hadi £31m, Adam Lallana wa Southampton
aliyekwenda Liverpool kwa £25m Dejan Lovren wa Southampton kwenda
Liverpool kwa £20m, Lazar Markovic kutoka Benfica kwenda Liverpool kwa
£20m
No comments:
Post a Comment